Ijumaa 28 Novemba 2025 - 07:39
Daima Jione Kuwa ni Mwenye Mapungufu

Hawza/ Kuona matendo mema kuwa makubwa na kuyafanya makosa na madhambi yaonekane kuwa ni madogo, kunaweza kuwa kikwazo katika njia ya ucha-Mungu wa mwanadamu; kwa hiyo, usia wa Maa’sumina (amani iwe juu yao) katika jambo hili unaweza kuwa ni muongozo sahihi.

Shirika la Habari la Hawza - Imam Zaynul-‘Abidin (amani iwe juu yake) anamsemesha Mwenyezi Mungu kwa maneno haya:

«اللَّهُمَّ ... أَلْبِسْنِی زِینَةَ الْمُتَّقِینَ، فِی ... اسْتِقْلَالِ الْخَیرِ وَإِنْ کثُرَ مِنْ قَوْلِی وَفِعْلِی، وَاسْتِکثَارِ الشَّرِّ وَإِنْ قَلَّ مِنْ قَوْلِی وَفِعْلِی.»

Ewe Mola! … nivishe mimi pambo la watu wa taqwa katika ‘kuona wema wangu kuwa mdogo katika maneno na matendo yangu, hata kama ni mwingi, na kuyaona mabaya yangu kuwa makubwa katika maneno na matendo yangu hata kama ni machache.’ (1)

Sherehe:

Kitu kinachoweza katika njia ya ucha-Mungu kikawa kama janga linaloharibu na kuangamiza amali zote za kiroho za mwanadamu, na kikamsababishia asimame au hata arudi nyuma katika njia ya kumtumikia Mwenyezi Mungu, ni pale mtu anapoyafanya matendo yake mema yaonekane kuwa ni makubwa machoni pake, huku akiyafanya makosa yake yaonekane kuwa ni madogo.

Iwapo tutauchukulia ulimwengu wote kuwa ni mahudhurio ya Mwenyezi Mungu na daima tukajione kuwa tupo mbele ya uwepo Wake; na iwapo tutamchukulia Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Mmiliki wa kila tulicho nacho na tusicho nacho, kamwe hatutaangukia katika janga hili.

Imam Kadhim (amani iwe juu yake) katika nasaha aliyompa mmoja wa wanawe alisema:


«یَا بُنَیَّ عَلَیْکَ بِالْجِدِّ لاَ تُخْرِجَنَّ نَفْسَکَ مِنْ حَدِّ اَلتَّقْصِیرِ فِی عِبَادَةِ اَللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ وَطَاعَتِهِ فَإِنَّ اَللَّهَ لاَ یُعْبَدُ حَقَّ عِبَادَتِهِ.»

“Ewe mwanangu! Jilazimishe kufanya bidii kubwa, na usijiondoe katika mipaka ya kujiona mwenye kasoro katika ibada na kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani Mwenyezi Mungu haabudiwi vile inavyopaswa aabudiwe.” (2)

Kwa hiyo, Imam Sadiq (amani iwe juu yake) ametusisitizia kwa namna hii:


«أَکْثِرْ مِنْ أَنْ تَقُولَ ... لاَ تُخْرِجْنِی مِنَ اَلتَّقْصِیرِ.»

“Kithirisheni kusema: Ewe Mola! Usiniondoe katika hali ya kujiona mwenye kasoro.”

Akaulizwa Imam kuhusu maana ya kauli: “Usiniondoe katika hali ya kujiona mwenye kasoro”?

Imam akajibu:

«کُلُّ عَمَلٍ تُرِیدُ بِهِ اَللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ فَکُنْ فِیهِ مُقَصِّراً عِنْدَ نَفْسِکَ فَإِنَّ اَلنَّاسَ کُلَّهُمْ فِی أَعْمَالِهِم فِیمَا بَیْنَهُمْ وَبَیْنَ اَللَّهِ مُقَصِّرُونَ.»

“Kila tendo unalolifanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, jione kuwa wewe ni mwenye kasoro katika kulitekeleza, kwa sababu watu wote katika matendo yao kati yao na Mwenyezi Mungu ni wenye kasoro.” (3)

Nukuu za rejea (Tanbihi):
1. Sahifa Sajjadiyya, Dua ya ishirini (Makarimul Akhlaq).
2. Wasaa’ilu-sh-Shi‘a, Juzuu ya 1, Ukurasa 95.
3. Usulu-l-Kaafi, Juzuu ya 2, Ukurasa 73.

Imeandaliwa katika Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha